- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
KIKAO CHA WADAU WA ELIMU WILAYA YA CHEMBA CHAFANYIKA TAREHE 05/01/2018.
Na Shani Amanzi,
Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe.Simon Odunga amewataka Watumishi wa Umma kutimiza wajibu wao maofisini na kuachana na kasumba ya kukimbia kazini kwa changamoto wanazozipata badala yake waboreshe mikakati waliyonayo ya kiutendaji ili kuweza kufikia tija ya kuwa na elimu bora siyo bora elimu shuleni katika Wilaya ya Chemba.
Mhe.Odunga aliongeza “tuheshimu kazi zetu, nidhamu iwepo kwenye kazi, hatuwezi kuwa na Viongozi wa Idara halafu hatufanyi vizuri shuleni kama Serikali tunahakikisha tunalinda Usalama wa Watumishi wa Serikali na nyie Watumishi mnapaswa kuwa makini na jamii inayowazunguka na msijihusishe na mambo yasiyo ya msingi yakawachafua ’’
Aidha Mhe.Odunga amesema lazima mwaka huu waingie mkataba na Waratibu Elimu Kata ambao kwa sasa ni (Maafisa Elimu Kata) ili waone tofauti kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka 2018 na utaratibu wa kuwapa chakula cha mchana shuleni wanafunzi unatakiwa kurudi katika Shule za Msingi na Sekondari.
Kwa upande wa Afisa Elimu Msingi Ndg.Modest Tarimo amesema pamoja na sababu nyingine, uhaba wa Walimu, upungufu wa madarasa, nyumba za Walimu na Matundu ya vyoo katika Shule za Msingi zimesababisha Wilaya ya Chemba kupata wastani wa asilimia 52 kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka 2017 na kuwa ya mwisho kimkoa kati ya Wilaya 08.
“ Mwaka 2018 malengo ni kufaulisha kwa asilimia 80 katika ngazi ya Wilaya na asilimia 90 kwa upande wa Shule na kata ikiwa ni pamoja na kupunguza daraja D na E kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa”alisisitiza Ndg. Tarimo.
Naye Kaimu Afisa Elimu Sekondari Ndg. Hausi Mkwachu amesema kuna upungufu wa vitabu vya kiada na ziada hususani vya masomo ya sanaa na upungufu wa Walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati hivyo kusababisha Wilaya ya Chemba kupata wastani wa asilimia 54 katika matokeo ya kidato cha IV mwaka 2016 lakini kwa upande wa kidato cha VI mwaka 2017 wilaya ya Chemba ilipata asilimia 100 na kuwa ya kwanza kimkoa.
Pia Mbunge wa jimbo la Chemba Mhe. Juma Nkamia aliongeza kwa kusema “ili kuboresha ufaulu kwa Wanafunzi inatakiwa kutoa Elimu kwa Wananchi kabla hatujawaomba michango kwa ajili ya maendeleo shuleni kwasababu kuna dhana waliyonayo kuwa Elimu ni bure”.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Chemba Dkt.Semastatus amesema “Kamati za shule, bodi za shule, Vikao vya WDC, na Mikutano ya kijiji iwe na agenda ya Elimu katika vikao vyao ili kuzungumzia changamoto za Elimu katika shule zao na kuzitatua”.
Dkt.Mashimba amesema kumekuwepo na Wadau wengi wa Elimu lakini Wafanyakazi wa Elimu wasitumie vigezo vya fedha za miradi kuwepo au kutokuwepo ndiyo sababu ya kukwama maendeleo ya shule za msingi na sekondari wilayani bali wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo iliyopo.
Kikao cha Wadau wa Elimu kimehusisha Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Chemba ambaye ni Mwenyekiti wa Kikao hicho, Katibu Tawala, Mheshimiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chemba, Mheshimiwa Mbunge wa jimbo la Chemba, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chemba, waheshimiwa Madiwani wa Chemba, Wathibiti ubora wa Shule, Chama cha Walimu, Waratibu Elimu, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Wakuu wa Idara kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chemba .
Chemba District Council
Sanduku la Posta: 830 CHEMBA
Simu ya Mezani: 0262360175
Simu ya Mkononi: 0765980765
Barua pepe: ded@chembadc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chemba . Haki zote zimehifadhiwa.