- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
"Maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo yana umuhimu wake katika jamii, yanamjenga mtoto kiakili na kimwili, na humuepusha mtoto na hali ya udumavu, Mtoto akiwa mdumavu hali ya utendaji wake na kufikiria inakua hairidhishi"
Hayo yamebainishwa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chemba Dkt.Marko Mgonja wakati akizingumza na akinamama waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji yaliyofanyika katika kituo cha huduma ya Mama na Mtoto kilichopo kijiji cha Mirambo Kata ya Goima Wilaya ya Chemba.
"Afya ya mama na mtoto ni muhimu sana, Sisi Sekta ya afya huwa tunatoa maelekezo kwamba mama anapojihisi ana ujauzito anatakiwa chini ya miezi mitatu yeye na mwenza wake ahudhurie kiliniki ili apate mafunzo juu ya namna bora ya kulea mimba ili mtoto atakayezaliwa awe na afya bora na baada ya kujifungua mama anaelekezwa namna ya kumnyonyesha mtoto wake" amesema Dkt. Mgonja
Aidha, Mganga Mkuu huyo amezungumzia suala uzazi wa mpango na kuwasihi akina mama kuwa ili mtoto aweze kunyonya vizuri anahitaji muda wa kuwa karibu na mama yake hivyo amewasihi akina mama kuzingatia njia za uzazi wa mpango ili mtoto apate haki yake ya msingi ya kunyonya vizuri na kukua vizuri.
"Mama anayenyonyesha au mwenye ujauzito anahitaji faraja, anahitaji kupumzika na apunguziwe kazi, hivyo hili ni suala La jamii nzima tushirikiane kwa pamoja kuhakikisha mama anayenyonyesha anapata muda wa kutosha wa kumnyonyesha mtoto" Amesema Dkt. Mgonja.
Dkt.Mgonja pia amewahamasisha kina mama wa Mirambo kujiunga katika vikundi na kuchangamkia fursa ya mikopo ya 10% ya Vijana, Wanawake na Watu wenye ulemavu inayotolewa na Halmashauri ili waweze kufanya shughuli mbalimbali zitakazowaingizia kipato na kujiimarisha kiuchumi.
Hata hivyo Dkt. Mgonja amewasihi kina mama kuepuka kujifungulia nyumbani, au kwa Wakunga wa Jadi na badala yake watumie Vituo vya huduma za afya kwa usalama zaidi wa mama na Mtoto na kuongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha vituo vya huduma za afya ili kuhakikisha Jamii inakua salama kwa kupata huduma bora za afya.
Akihitimisha maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji Afisa lishe wa Wilaya Bi Faith Temu ameshukuru shirika La Compassion pamoja na Viongozi wa dini Kijiji cha Mirambo kwa kuunga mkono Juhudi za Serikali ili kuimarisha huduma ya mama na mtoto na kuwaomba kina mama wote waliohudhuria kilele cha wiki ya unyonyeshaji kuwa mabalozi kwa kina mama wengine katika maeneo yao kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji ili Wilaya ya Chemba iweze kuwa na kizazi chenye afya bora.
Thamini Unyonyeshaji; weka mazingira wezeshi kwa Mama na Mtoto
#Lishe ya mwanao, mafanikio yake# Kujaza tumbo si lishe, jali unachomlisha.
Chemba District Council
Sanduku la Posta: 830 CHEMBA
Simu ya Mezani: 0262360175
Simu ya Mkononi: 0765980765
Barua pepe: ded@chembadc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chemba . Haki zote zimehifadhiwa.