- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkurugenzi Mtendajiwa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Ndugu Hassan Mnyika ametoa pongezi hizo katika hafla fupi ya kuwapongeza Walimu wa shule zilizofanya vizuri katika mtihani wa kidato cha sita 2025 iliyofanyika Julai 16, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
"Kwa dhati ya moyo wangu leo nimefurahi sana, nawapongeza sana,ninawashukuru sana, mmenivika nguo na mmeniheshimisha,ninawaahidi kushirikiana nanyi bega kwa bega ili tuweze kufanya vizuri zaidi" amesema Mkurugenzi Mnyika.
Ndugu Mnyika amewaomba Walimu hao pamoja na mazingira magumu waliyonayo wasikate tamaa, waendelee kujitumi na mafanikio haya waliyoyapata wayashikilie na walenge kupata ufaulu wa juu zaidi, wafanye kila linalowezekana ambapo pia amewaahidi ushirikiano na kuwatembelea katika maeneo yao mara kwa mara ili waweze kujadili kwa pamoja mambo muhimu yahusuyo sekta hiyo muhimu ya elimu.
Mapema akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa divisheni ya elimu ya Sekondari Bi. Jeanimina Mtitu amesema kuwa ufaulu wa juu ndio mpango mzima hivyo amewataka Walimu hao wajikite katika kuangalia ubora wa ufaulu ambapo ameongeza kuwa matamanio yake mwakani 2026 ni kuifanya Chemba ichukue nafasi tatu za mwanzo Kimkoa.
"Ndugu zangu tumekutana hapa Leo kwa jambo Moja tu kufurahi, kula na kunywa, mwakani tunaweza kwenda mbali zaidi hata Zanzibar kupongezana kama tutafanya vizuri zaidi" amesema Bi Jeanimina
Kwa upande wake Afisa taaluma Sekondari Bi Bernadetha Akaro amesema kuwa ufaulu kwa Shule unaonesha kuwa Shule ya Sekondari Msakwalo inaongoza kwa kuwa na wastani wa alama za gredi (GPA) ya 1.8669 ikifuatiwa na Shule ya Sekondari Soya ikiwa na GPA ya 2.3759 na Shule ya Sekondari ya Mondo imeshika nafasi tatu ikiwa na GPA ya 2.7469 Kiwilaya.
Sambamba na hilo Mtaaluma huyo amesema kuwa katika matokeo hayo ya kidato cha sita 2025 jumla ya Wanafunzi 307 wamepata daraja La kwanza, 114 daraja la pili, Wanafunzi 40 wamepata daraja La tatu na Mwanafunzi 1 amepata daraja la 4.
Aidha, Bi Bernadetha amebainisha kuwa Shule ya Sekondari Msakwalo kwa mwakani 2024 ilipata ufaulu wa GPA ya 2.0527 wakati mwaka 2025 ubora wa ufaulu ni 1.8669, Shule hii Kimkoa imeshika nafasi ya 3 wakati mwaka 2024 ilishika pia nafasi ya 3 ambapo Kitaifa imeshika nafasi ya 62.
Bi Bernadetha amesema kuwa kiujumla Halmashauri ya Wilaya ya Chemba imekua ya kwanza Kimkoa kwa miaka miwili mfululizo, mwaka 2024 ubora wa ufaulu ulikua ni 2.3393 na mwaka 2025 ubora wa ufaulu ni 2.3299.
Akihitimisha taarifa ya tathimini ya matokeo ya kidato cha sita 2025 Mtaaluma Huyo ameeleza kuwa mafanikio hayo mazuri yametokana na jitihada za Walimu ambapo wametoa ushirikiano na kujituma katika kutekeleza mikakati yote iliyowekwa ili kufanikisha lengo la Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha viwango vya ufaulu katika sekta hiyo muhimu ya Elimu.
Chemba District Council
Sanduku la Posta: 830 CHEMBA
Simu ya Mezani: 0262360175
Simu ya Mkononi: 0765980765
Barua pepe: ded@chembadc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chemba . Haki zote zimehifadhiwa.